|
Mratibu wa AMANI KWANZA Muhidin Issa Michuzi akiwa na wanamuziki nyota wa Tanzania - Cassim Mganga wa Bongo Fleva na Hassan Rehani Bitchuka 'Stereo' katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es salaam Ijuma Septemba 18, 2015. Hii ikiwa ni mwanzo mzuri na mwendelezo wa dhamira ya kundi la AMANI KWANZA la kuunganisha vipaji vya kale na vya sasa. |
Nyota wa Bongo Fleva Cassim Mganga akiwa na gwiji la uimbaji Tanzania Hassan Rehani Bitchuka 'Stereo'
Awali ilianza kama kundi la wanamuziki wakongwe nchini Tanzania waliojikusanya ili kutunga wimbo wa kuhamasisha amani wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, na baada ya uchaguzi huo.
Walipofanikisha hilo, wanamuziki hao wakakaa na kutafakari. Je, baada ya wimbo huu nini kifuatie?
Ndipo likaja wazo la kuudumisha umoja huo kwa kuanzisha kunzi la wanamuziki, wakongwe na vijana, ili kuweka sawa mustakabali wa muziki wa Tanzania.
Hivyo azma mama ya AMANI KWANZA GROUP ni kuwaunganisha wanamuziki wakongwe na vijana ili kuziba ombwe kubwa lililopo, ambapo kwayo kumesababisha mfarakano usio wa lazima, kwani duniani kote wanamuziki wakongwe na vijana sasa wanaungana na kufanya kazi pamoja. Sembuse Tanzania?
Hayawai hayawi sasa yamekuwa. Wanamuziki wakongwe sasa wameamka na kuamua kurithisha vipaji vyao kwa wanamuziki vijana, maarufu kama BONGO FLEVA. Makubaliano ni kwamba kuanzia sasa wanamuziki wakongwe watashikamana na wanamuziki vijana ili kukuza tasnia hii.
Hakuna safari isiyo na changamoto zake. Ile sintofahamu iliyopo baina ya wanamuziki wakongwe na vijana lazima itajitokeza sana. Upande mmoja ukisema wazee ni wazee na wakati wao umepita, na vijana wakisema wakongwe hawana jipya, hiyo ikiwa ni KOSA moja kubwa sana ambalo wanamuzki wa Tanzania wanafanya.
Piga ua, lakini kila upande hapo unategemea mwenzake. Muungano huu wa wakongwe na vijana unaashiria mambo mazuri kwa tasnia ya muziki Tanzania. Kilichokosekana awali sasa kimepatikana.
Wakongwe na vijana watakuwa kitu kimoja kwa maslahi ya Taifa la Tanzania.
IDUMU AMANI KWANZA!